Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, utawala wa Kizayuni ulitangaza siku ya Jumanne kuwa umepokea mabaki ya mwili wa Itay Chen, mateka wa mwisho mwenye uraia wa pande mbili -Marekani na Israel- aliyekuwa akishikiliwa katika Ukanda wa Gaza. Hatua hii ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yaliyotekelezwa mwezi Oktoba uliopita kwa upatanishi wa Marekani.
Kwa mujibu wa maafisa wa Israel, jeneza lililokuwa na mabaki ya Chen lilipokelewa kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu ndani ya Gaza na kisha kupelekwa katika Kituo cha Kitaifa cha Uchunguzi wa Vifo, ambapo utambulisho wake ulithibitishwa rasmi. Baada ya uthibitisho huo, imebainika kuwa mabaki ya mateka saba pekee ndio yaliyosalia ndani ya Gaza.
Itay Chen, aliyekuwa sershanti wa kwanza katika jeshi la Israel, alikuwa akihudumu mpakani mwa Gaza wakati wa shambulio la Hamas tarehe 7 Oktoba 2023. Kwa mujibu wa jeshi, aliwaawa katika mapigano na mwili wake ulihamishwa kupelekwa Gaza.
Makabidhiano haya yalifanyika baada ya Hamas kukabidhi miili ya mateka watatu wengine siku ya Jumapili. Awali, siku ya Alhamisi, Hamas pia ilikuwa imetoa mabaki ya mateka wawili waliotambulika kwa majina ya Amiram Cooper (miaka 84) na Sahar Baruch (miaka 25).
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yaliyopatikana kwa upatanishi wa Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, yalikuwa yamekabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo tukio la tarehe 28 Oktoba ambapo Hamas ilisema imekabidhi mabaki ya watu watatu waliokufa, lakini Israel ilishindwa kuthibitisha utambulisho wao.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alijibu tukio hilo kwa kusema: “Hamas inajaribu kutudanganya sisi, Marekani na dunia nzima.”
Baada ya kauli hiyo, Netanyahu alitoa amri ya mashambulizi makali dhidi ya Gaza, ambayo yalisababisha vifo vya angalau Wapalestina 104, wakiwemo watoto kadhaa, na siku hiyo ilitajwa kuwa siku yenye umwagaji damu zaidi tangu kuanza kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Your Comment